MKUU wa wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro, amekasirishwa na kitendo kili cha wananchi wa kijiji cha Mwang’halanga kilichopo kata ya Usanda ndani ya Wilaya ya Shinyanga kuchangishwa fedha za kupaua jengo la Zahanati ya kijiji hicho Shilingi Milioni 11.7 lakini fedha hizo zimeshindwa kutekeleza ujenzi huo, Sababu mpaka sasa jengo hilo halijapauliwa.
Mtatiro amesikitishwa na kitendo hicho wakati akisikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Mwang’halanga na kuzitatua siku ya Januari 15, 2025 , ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake ya kufikia kila kijiji kusikiliza kero za wananchi, ambapo amefika pia kijiji cha Singita na Manyada.
DC Mtatiro amesema kuwa kwa changamoto ya Wananchi wa kijiji cha Mwang’halanga kushindwa kupauliwa Zahanati yao na wakati wamechangishwa fedha kila Kaya Sh.28,000 na kuna Kaya 418 sawa na sh.milioni 11.7, lakini fedha hizo hadi leo hazijapauwa jengo hilo la Zahanati,na kwamba huko ni kucheza na pesa za wananchi.
“Acheni mchezo na pesa za wananchi, Dunia gani utapata wananchi wanachangishana fedha hadi kutimia Shilingi Milioni 11 utawapata wapi, leo mnakuja kuniambia zimekwama kwenye mfumo wa NeST hili hapana,” amesema DC Mtatiro.
“Haiwezekani Mtendaji wa Kijijji amechangisha pesa za wananchi na pesa hizo akaziweka kwenye Akaunti ya kijiji kwa uaminifu kabisa pamoja na fedha za mfuko wa jimbo Sh.milioni 3 jumla milioni 14, na hadi sasa jengo hilo halijapauliwa na kunieleza sababu ni mfumo wa NesT huku ni kucheza na pesa za wananchi,” ameongeza DC Mtatiro.
Aidha, ameagiza Menejimenti ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, kwamba ifikapo tarehe 27/1/2025 kuwa siku hiyo ni siku ya kwenda kupaua jengo la Zahanati hiyo na yeye atafika hapo pamoja na Kamati yake ya ulinzi na usalama kupaua pamoja na wananchi.

Akizungumzia suala hilo Mtendaji wa kijiji cha Mwang’halanga Helena Kayagila, amesema wananchi wa kijiji hicho walichangishwa fedha hizo Agosti 30 mwaka jana, pamoja na kutolewa Sh.milioni 3 katika mfuko wa jimbo, na yeye akaziweka kwenye akaunti ya kijiji Sh.milioni 14 na kwamba kilicho kwamisha fedha hizo kutolewa ni tatizo la mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya umma NeST.
Diwani wa Samuye John Ngengeshi, naye akizungumza kwenye mkutano huo, amesema kwamba ukwamishaji wa fedha hizo za wananchi kupauwa zahanati ya kijiji hicho linatokana na kukwama kwa mfumo wa NeST, sababu ambayo mkuu wa wilaya hakukubaliana nayo.

Nao baadhi ya wanakijiji wa Mwang’halanga akiwamo Manase Elias, awali walisema kama pesa zao walizochanga zimeshindwa kupaua Zahanati yao, ni vyema wakarudishiwa pesa hizo, na kwamba wao waliridhia kuchangishana ili wapate huduma za matibabu karibu na makazi yao lakini wanaona kimya.

Katika ziara hiyo ya Mkuu wa wilaya amesikiliza kero za wananchi ikiwamo changamoto ya ukosefu wa maji, ubovu wa barabara, kutokamilika maboma ya zahanati, umeme, pamoja na migogoro ya ardhi, huku akiagiza wazazi kupeleka watoto wa shule na kwamba mwisho itakuwa ijumaa na baada ya hapo zoezi la ukamataji linaanza.
