Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt. Jafar Seif amesema Serikali imeunda mfumo wa kielektroniki wa utoaji na usimamizi wa mikopo ambapo kila mwombaji anautumia kuomba mkopo, ikiwa ni hatua ya kuweka uwazi na uwajibikaji katika kila hatua ya utoaji wa mikopo, usimamizi na marejesho.
Dkt. Seif amesema hayo leo Aprili 8, 2026 Bungeni Jijini Dodoma kwa Niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wakati akijibu swali la Mhe. Devotha Daniel Mburarugaba (Viti Maalum) aliyetaka kujua Serikali imechukua hatua gani katika kuhakikisha usimamizi, utoaji na urejeshaji wa Mikopo 10% ya Halmashauri unakuwa wazi na unawafikia walengwa.
“Mfumo huo wa kieletroniki utatumika kuweka uwazi katika mchakato wa uombaji na utoaji wa mikopo, lakini pia unatumika katika usimamizi wa shughuli za vikundi pamoja na kufuatilia marejesho,” amesisitiza Dkt. Seif.

Dkt. Seif ameongeza kuwa, serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha mchakato mzima wa usimamizi, utoaji na urejeshaji wa mikopo unakuwa wazi na usawa, Utaratibu ambao umeainishwa kwenye kanuni na katika mwongozo ambao halmashauri zote nchini zimepewa.
Aidha, Dkt. Seif ameanisha kuwa, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha kunakuwa naÿ uwazi katika uombaji na utoaji wa mikopo kama kanuni na miongozo inavyoelekeza.