Na Daniel Gahu – Katavi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, ameongoza sherehe ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba na mazao mengine kwa mwaka 2025/26, hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Kapalala (Nsimbo)na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, vyama vya ushirika, wakulima, na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo.
RC Mrindoko amewataka wakuu wa wilaya kuhakikisha kuwa mauzo ya mazao yote yanapitia kwenye vituo rasmi vilivyoidhinishwa na serikali pamoja na mifumo rasmi ya kibiashara nakusisitiza kuwa utaratibu huo unasaidia kudhibiti uuzaji holela wa mazao, huku ukihakikisha wakulima wanabaki na akiba ya chakula na kuuza ziada pekee.

Ameeleza kuwa kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS), mazao ya pamba na tumbaku yanapaswa kusimamiwa kwa umakini mkubwa kwani kumekuwepo na matukio ya hujuma kutoka kwa baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wanaokiuka taratibu za kilimo cha mkataba na kuingia mikataba isiyo rasmi na wakulima.
Amewaelekeza wakuu wa wilaya kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa kilimo cha mkataba kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, ili kuwalinda wakulima dhidi ya unyonyaji unaofanywa na watu binafsi wanaotoa mikopo ya pembejeo kisha kujinufaisha na mazao ya wakulima.

Amefafanua kuwa mkoa wa Katavi umeungana na mikoa mingine katika kuanza kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa zao la ufuta katika msimu huu wa 2025/26 na kusema kuwa mfumo huo uliwahi kujaribiwa mwaka 2019/20 lakini ukakumbwa na changamoto zilizofanya utekelezaji usiendelee. Hata hivyo, kutokana na mafanikio yanayoonekana katika mikoa mingine, Katavi imeamua kurejea kwenye mfumo huo kwa lengo la kuhakikisha wakulima wananufaika kupitia usalama wa soko na ongezeko la thamani ya mazao yao.

Mwakilishi kutoka Bodi ya Pamba, Bugelaha Filbert, amesema kuwa mkulima ili aweze kufaidika na kilimo chake ni lazima azalishe kwa tija, kwa maana ya kupata mavuno mengi katika eneo dogo na amesisitiza kuwa Bodi ya Pamba inaendelea kusisitiza matumizi ya mbolea na mbegu bora sambamba na matunzo sahihi ya zao la pamba.