Shirika la Habari la Uingereza (BBC) limeripoti kuwa nyangumi mmoja mwenye nundu amesafiri kwa umbali wa kilometa 13,000 kutoka Colombia na kufika Tanzania kwa ajili ya kutafuta wenza na kujilinda na mabadiliko ya tabianchi.
Mtaalamu kutoka kwenye programu ya mamalia wa baharini nchini Tanzania, Ekaterina Kalashnikova amesema tukio hilo ni la kushangaza na la kipekee hata kwa aina hii ya wanyama wanaohama sana.
Wanasayansi wanasema alionekana Bahari ya Pasifiki karibu na nchi ya Colombia mwaka 2017, kisha kuzuka tena miaka kadhaa baadaye kisiwani Zanzibar katika Bahari Hindi.
Wataalamu wanaamini kuwa safari hii ya umbali wa kilomita 13,000 inaweza kuwa imesababishwa na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kupungua kwa hifadhi za chakula au safari ya kutafuta wenza,” imeripoti BBC.
Nyangumi huyo mwanaume pia aliwahi kuonekana katika pwani ya Pasifiki nchini Colombia mwaka 2013.Alitambuliwa tena katika eneo hilo mwaka 2017 na kuonekana kando ya Bahari ya Hindi visiwani Zanzibar mwaka 2022.