Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, imemhukumu kwenda jela miaka 23 Amos Benard Mtinange maarufu kwa jina la Meja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ujangili wa Twiga na kuuza nyama za Twiga kinyume cha sheria.
Meja alikamatwa April 21 mwaka huu wa 2013, saa 11 jioni maeneo ya mfulwang’ombe kwenye Kambi ya samaki Kijiji cha Vilima vitatu, ndani ya eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori ya Burunge wilayani Babati mkoani Manyara baada ya kusakwa muda mrefu kutokana na kujihusisha na ujangili wa Twiga na kufanya biashara ya nyama za Twiga.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Babati, mkoa wa Manyara, Victor Kimario amesema, mahakama imemtia hatiani Meja baada ya kujiridhisha pasi na shaka kuwa amekuwa akijihusisha na ujangili wa Twiga na kuuza nyama za Twiga.