Mchambuzi nguli wa michezo nchini, Edo Kumwembe ameonesha kusikitishwa na kauli aliyoitoa Kocha mkuu wa klabu ya Kagera Sugar FC, Mecky Mexime jana juu ya Kocha wa Simba SC, Abdelhak Benchikha kuelekea mechi yao ya leo, akisema ni kauli ya kibaguzi.
Kumwembe ameandika kwenye mtandao wake wa Instagram hivi:”Jana nimesikitika sana wakati rafiki yangu Mecky Mexime akimpuuza kocha wa Simba, Benchikha kwa kudai “Basi tu kwa sababu yeye mweupe na anavaa kofia lakini mbinu zetu ni zile zile tu.
“Ameongea na watu wameona kawaida, leo Simba akimfunga Kagera halafu Benchikha akasema “kocha wao hana uwezo kwanza ni mweusi na ana upara”, Wabongo wote tutakuja juu kwamba Benchikha ni mbaguzi.
“Tatizo letu tunadhani ubaguzi ni mtu mweupe kumbagua mweusi kwa rangi yake, jana Benchikha kabaguliwa kwa muktadha wa alichoongea Mecky, Kama Mecky angemaanisha kuwa Benchikha anabebwa kutokana na kuwa kocha wa kigeni, hapo sawa, lakini issue sio weupe.
“Lakini hata kwa muktadha wa mafanikio tujifunze kwa waliotuzidi, Benchikha ana mataji mengi tena akichukua katika nchi ambayo imetuacha mbali kisoka. Last season tu amechukua confederation,” mwisho wa kunukuu alichokiandika mchambuzi Edo Kumwembe.