MEATU: WAKAZI 2,600 WA VIJIJI VINAVYOZUNGUKA HIFADHI KUPATIWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI

Na Saada Almasi – Simiyu.

Zaidi ya wakazi 2600 kutoka katika vijiji 16 vinavyozunguka maeneo ya Hifadhi ya pori la akiba la Maswa wilayani Meatu mkoani Simiyu watanufaika na mafunzo ya ujasiriamali kutoka shirika la Hand in Hand lililowekeza zaidi ya shilingi bilioni 1.6 ili kuwaelekeza namna ya kutumia uoto wa asili na kujitengenezea fedha kutokana na vitu vinavyopatikana katika mazingira wanayoishi

Akifungua mafunzo hayo mkuu wa wilaya ya Meatu Fauzia Ngatumbura amesema kuwa hatua hiyo inakwenda kupunguza uharibifu wa mazingira ya hifadhi kwani kila mmoja atakuwa na shughuli ya uzalishaji anayoifanya inayotokana na mazingira anayoishi hivyo wanatakiwa kufuata miongozo na taratibu za kiserikali ili kufanikisha.

“twende tukasimamie taratibu na miongozo ya serikali katika utekelezaji wa hii miradi ya kimaendeleo kwa faida ya kila mmoja kwani uharibifu wa mazingira ya hifadhi yanasababishwa na watu kutokuwa na kitu mbadala cha kufanya kujiingizia kipato lakini sasa uzalishaji utafanyika kwa kutumia mazingira ya mtu anayoishi”Dc Fauzia

Afisa mradi huo Novatus Njaala amesema kuwa hivi karibuni kumekuwa na matukio ya kujirudia ya uvamizi wa Wanyama kama tembo katika makazi ya watu na kuharibu mazao yao hivyo kuanzisha miradi kama ufugaji wa nyuki licha ya kuwapa asali ya biashara bali yataondoa adha ya uvamizi kwani nyuki ni adui wa Tembo.

 “hawa wanyama wanavamia mashamba ya wakazi kwa kutafuta vyakula na wakishavuruga shamba inakuwa hasara kwa mkulima lakini kufuga nyuki mkulima atapata asali kwa biashara lakini huyu tembo hatosogea maeneo hayo kuharibu kwa kuwa hapatani na nyuki,” amesema Novatus.

Naye meneja maendeleo ya jamii kutoka shirika la uhifadi la Fredkin Sylvester Sadok amewataka wakazi hao kuwapa ushirikiano ili kwa pamoja wapunguze ujangili kwa kutengeneza bidhaa zitakazo ingia sokoni na kuwapa faida kiuchumi.

“Maisha ya utafutaji ndiyo yanapelekea ujangili kwa lengo la kupata nyama za kuuza na matumizi binafsi sasa tunaomba ushirikiano kwa jamii zote ili kupunguza ujangili inafaa tutengeneze bidhaa kutokana na mazingira yetu ili yatupe faida kiuchumi tuachane na ujangili,” amesema Sylvester.

Jambo fm imezungumza na Emmanuel Fabian mtendaji wa kata ya Butuli ambaye amesema kuwa vijana watainuka kiuchumi na hatimaye ule utegemezi utapungua katika jamii na kila mtu atakuwa na jambo la kufanya na baada ya muda watavuka kutoka sehemu moja kwenda nyingine kimaendeleo.

Sambamba na hilo Mary Mwijanja mtendaji wa kata ya Mwakisando  amesema kuwa uoto wa asili ulitumika na kuharibiwa vibaya kwa vitendo vya ukataji miti kwa ujenzi na kuni lakini sasa jamii itaulinda kwa kuwa uoto huo utakuwa ndiyo sababu ya mapato yao.

“hapo awali jamii ilikuwa inaharibu uoto wa asili kwa kukata miti kujenga nyumba na matumizi ya kuni sasa tukianza kuutumia uoto viziri ukatunufaisha tutaulinda kwa kuwa umeshageuka chanzo cha kutuingizia kipato niseme tu ushiriki wa kila mtu utaleta manufaa makubwa,” amesema Mary.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *