Mchungaji mmoja nchini Kenya anachunguzwa baada ya madai kwamba yeye na wazee wengine wa kanisa lake waliwanyanyasa kingono wanawake na wasichana kadhaa.
Kesi hiyo ilibainika baada ya kanisa linaloendeshwa na Daniel Mururu katika kaunti ya Meru, katikati mwa Kenya, kuchomwa moto na wakazi wenye hasira mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kulingana na ripoti ya polisi ya Jumatatu ya wiki hii,Mururu ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Pentekoste la Afrika Mashariki nchini Kenya pamoja na wazee wa kanisa na washemasi, wanatuhumiwa kwa vitendo vya udhalilishaji vikiwemo kuwavua nguo, kuwaacha wanawake uchi, kuwanyoa nywele sehemu zao za siri na kufanya nao ngono.
Zaidi ya wanawake na wasichana saba wenye umri kati ya miaka 17 hadi 70 wanadaiwa walidhulumiwa kingono ikiwemo msichana wa shule mwenye umri wa miaka 17 ambaye alipata ujauzitona taarifa ya polisi imeoneza kwamba uchunguzi wao wa awali ulibaini kwamba Mururu alikuwa akiendesha dhehebu ambalo liliwafanya wafuasi wake kuwa na msimamo mkali.
Wanachama wa kanisa hilo walishawishiwa kufanya vitendo vya udhalilishaji kwa hofu ya matokeo kama vile magonjwa na utasa ikiwa watakaidi maagizo ya mchungaji katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya waumini wa kikristo ambayo imekuwa ikipambana kudhibiti makanisa na madhehebu yasiyo na uadilifu ambayo yanajihusisha na uhalifu.