Emanuel Karata (35) na mwenzake mmoja anayefahamika kwa jina la Basenga Matheo (59) wameshikiliwa na jeshi la polisi mkoani Pwani kwa kutengezeza tukio la kishirikina la kuanguka na ungo kanisani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, ACP Pius Lutumo amesema kuwa watu hao wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Lutumo amesema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 24 mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi kwenye kanisa hilo, ambapo Matheo aliahidiwa ujira wa Sh 50,000 kutekeleza tukio hilo ili kuongeza waumini na lengo la mchungaji na mtuhumiwa huyo ni kupata waumini zaidi kwa ajili ya kuongeza kipato.
Amesema kuwa Matheo alianguka na ungo na vifaa vyake vya kishirikina akiwa na wenzake sita wakati akisafiri kishirikina na kudondoka kanisani hapo jambo ambalo lilileta taharuki kubwa kwa waumini.
Aidha Kamanda amesema kuwa baada ya uchunguzi wamebaini kuwa tukio hilo ni la kutengeneza kwa lengo la kuwalaghai na kuwaadaa waumini na wananchi.
Ametoa onyo kwa watu wenye tamaa ya kupata kipato kwa haraka kwa kufanya ulaghai na kuacha mara moja na kuwataka waumini kuwa makini na watu hao wanaotaka kuharibu imani za kidini kwa tamaa ya kipato.