Wadau wa Michezo pamoja na watanzania kwa ujumla wameombwa kuchangia matibabu ya mchezaji wa zamani aliyewahi kuzitumikia kwa nyakati tofauti wa klabu za Yanga SC,Kagera Sugar, Moro United, Kahama United , 82 Rangers ya Shinyanga pamoja na Timu ya Taifa ya Tanzania kwa nyakati tofauti Karume Songoro ambaye anasumbuliwa na maradhi ya Saratani ya Misuli.
Akizungumza na Jambo Fm kwa niaba ya mchezaji huyo, msemaji wa familia ndugu Shareef Wakutampa ameleza kwamba hali yake kwasasa haiko sawa na anahitaji msaada wa hali na mali ili kufanikisha matibabu ya ugonjwa huo unaomsumbua na kubainisha kuwa kuwa dalili za ugonjwa unaomsumbua zilianza kuonekana mwishoni mwa mwezi Januari na jitihada za kumpeleka hospitali zilifanyika na alipofikishwa hospitali ya rufaa ya Bugando ndipo alipobainika kuwa na tatizo hilo.
Shareef amewaomba wapenda michezo pamoja na Watanzania wote kwa ujumla kusaidia matibabu ya mkongwe huyo wa soka katika mpira wa Tanzania kwa kiasi chochote watakachoguswa kwa kupitia namba 0755686722 na 0675304081 zilizosajiliwa kwa majina Karume Songoro Jumanne.
Karume Songoro anakumbukwa kama moja kati ya wachezaji wenye umbo kubwa na kasi waliowahi kucheza katika soka la Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipoanza kusakata soka na kufanikiwa kuvitumikia vilabu vya ligikuu ya Tanzania ambavyo ni Yanga,Kagera Suger, Moro United, Kahama United, Afrika Lyon, 82 Rangers ya Shinyanga, pamoja na Timu ya taifa ya ambayo moja kati ya mchezo wa kukumbukwa zaidi ni ule aliyoitumikia Tanzania katika mechi dhidi ya Zambia mnamo mwaka 2003 kabla ya kustaafu mwaka 2010 akiwa anaitumikia klabu ya African Lion.