Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busega mkoani Simiyu, Veronica Sayore amesimamishwa kazi kuanzia leo Septemba 22, 2023 ili kupisha uchunguzi.
Amri hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa baada ya kupokea malalamiko kuhusu utendaji kazi usioridhisha, kutokuwa na ushirikiano na viongozi wenzake pamoja na kutowashirikisha watendaji katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kutokana na tuhuma hizo, Waziri Mchengerwa amemwelekeza Katibu Mkuu Tamisemi kuunda timu ya uchunguzi wa mwenendo wa utendaji kazi wa mkurugenzi huyo pamoja na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega.
Aidha, Mchengerwa amewataka wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za Mitaa, kusimamia dhana ya ushirikishwaji wa viongozi, watendaji na wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuimarisha mahusiano mazuri baina ya viongozi na watendaji ili kujenga timu yenye umoja katika kutekeleza jukumu la kuwahudumia wananchi.