Wahitimu 222 wa Chuo cha Afya Exelent kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani, wamehimizwa kuzingatia maadili ya taaluma yao na kutumia ujuzi walioupata kutoa huduma bora kwa jamii, huku wakitakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na ufisadi vitakavyoweza kuharibu taswira ya sekta ya afya.
Wito huo umetolewa Februari 26, 2026 wakati wa mahafali ya saba ya chuo hicho, ambapo mgeni rasmi, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Subira Mgalu aliwakilishwa na msaidizi wake John Mrema.
Akizungumza kwa niaba ya mbunge huyo, Mrema amesema wahitimu wanapaswa kwenda kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za afya katika jamii kwa kuzingatia taaluma waliyoipata na kufanya kazi kwa uadilifu.

Amewataka wahitimu kuhakikisha wanatoa huduma kwa kuzingatia misingi ya taaluma ya afya na kuepuka vitendo vya rushwa vinavyoweza kudhoofisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Jamii inawategemea sana katika kuboresha huduma za afya, hivyo ni muhimu mkaitumikie taaluma yenu kwa uaminifu, uadilifu na kujituma, huku mkijiepusha na vitendo vya rushwa na ufisadi,” amesesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vyuo vya Exelent, Msaada Balula amesema pamoja na mafanikio yanayopatikana katika kutoa mafunzo ya afya, bado wanafunzi wengi wanakabiliwa na changamoto ya ada, jambo linalosababisha baadhi yao kushindwa kuendelea na masomo.

Ametoa wito kwa serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza wigo wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati ili kuwawezesha kumudu gharama za masomo na kuongeza idadi ya wataalamu wa afya nchini.
Mmoja wa wahitimu hao Peter Thomasy amesema elimu waliyoipata itawawezesha kuitumikia jamii kwa ustadi na weledi, huku akiwahimiza wahitimu wenzake kuendelea kujiendeleza kitaaluma ili kuongeza ujuzi zaidi.
Jumla ya wahitimu 222 walitunukiwa vyeti katika mahafali hayo ya saba ya Chuo cha Afya Exelent, wakitarajiwa kujiunga na sekta ya afya ili kusaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
