MBEGU ZA RUZUKU KUWANUFAISHA WAKULIMA SHINYANGA

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Serikali imetoa tani 192 za mbegu bora za mazao mchanganyiko zenye thamani ya Sh Bilioni 1.82 katika msimu wa mwaka 2025/2026 ambazo zitanunuliwa na kusambazwa kwa Wakulima katika Mkoa wa Shinyanga, ili kuwawezesha kuwa na kilimo chenye tija na kuwezesha kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa MKoa wa Shinyanga, Mboni Mhita wakati wa uzinduzi wa mpango wa Taifa wa ugawaji wa mbegu bora kwa wakulima msimu huu  wa kilimo mwaka 2025/2026,kupitia mamlaka ya udhibiti  wa nafaka na mazao mchanganyikao (COPRA) huku akianisha kuwa  mbegu bora ni ni msingi wa kilimo cha uhakika na kuimarisha uchumi wa mkulima.

Mkuu wa MKoa wa Shinyanga, Mboni Mhita.

Amesema, mbegu hizo zilizotolewa na serikali kupitia ruzuku ni kwa mazao ya ufuta tani 126,mbaazi tani 16,choroko tani 17,dengu tani 30 na soya tani 3, huku zao la choroko tani 3  mbegu ambazo  zimetolewa kupitia   mamlaka ya udhibiti wa nafaka na mazao mchanganyiko (COPRA).

“Wakulima watakao nufaika na mbegu hizo ni wale ambao wamejisajili kwenye mfumo wa ruzuku na mbegu hizi zitasambazwa kwa wakulima waliouza mazao yao kupitia masoko ya kidigital na itakuwa kwa njia ya masoko ya kidigitali yatakayofanyika kila halmashauri,” amesema RC Mboni.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewataka wakulima kuacha kuuza mazao yao kwenye mifumo isiyorasmi ambayo imekuwa ikiwaibia na kuikosesha serikali mapato kutokana na kukosa takwimu sahihi za mauzo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola amesema licha ya kutoa mbegu bora pia wakulima watapatiwa elimu ili kuwa na kilimo chenye tija ambacho kitamuwezesha kupata mavuno mengi zaidi na kukuza uchumi wao.

Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola.

Ameongeza kuwa, mpango huo unalenga kuwafikia wakulima waliouza mazao kupitia mfumo rasmi na kuhakikisha wakulima wanapata masoko na kuuza kwa bei nzuri,ambapo kwa mwaka huu wa 2025 wameuza tani laki 565,000 za mazao mchanganyiko na kupata zaidi ya Trioni moja.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghafla, Asangye Bangu amesema wamefarijika kuona wakulima wameanza kunufaika pamoja na wafanyabiashara na sasa wanaanza maandalizi na wakulima hadi mazazo yanapokomaa wanakuwa karibu.

Kwa upande wake Mkulima Daison Cherehani kutoka kijiji cha Shilabela, amesema mfumo wa stabadhi za ghala umewanufaisha kwani awali walikuwa wanaibiwa na walanguzi kwa kuuza kilo Sh 800 ambapo kwa mfumo huo wanauza Sh 1000 na wakati mwingine inaweza kuongezeka.

Mbegu hizo, pia zimegawiwa kwa Wakurugenzi katika halimashauri zote sita za mkoa wa Shinyanga, ili kuzisambaza kwa wakulima katika maeneo yao, kwa bei nafuu kupitia ruzuku iliyotolewa na serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *