
Iran imetangaza kuwa itafanya uchaguzi wa rais mnamo Juni 28, kufuatia kifo cha rais Ebrahim Rais na maafisa wengine katika ajali ya helikopta wakati mazishi yakitarajiwa kufanyika Jumanne ya leo.
Ripoti za vyombo vya habari vya taifa nchini Iran, zinasema kuwa tarehe hiyo ya uchaguzi, imeidhinishwa wakati wa mkutano wa wakuu wa mihimili mikuu ya serikali na kulingana na makubaliano ya awali ya baraza la ulinzi, iliamuliwa kuwa uchaguzi wa 14 wa urais utafanyika Juni 28.
Aidha Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, ametangaza siku tano za maombolezo na kumtaja makamu wa rais Mohammad Mokhaber kuwa anachukua majukumu ya rais wa mpito hadi uchaguzi utakapofanyika.

Maelfu ya waombolezaji wameendelea kumiminika katikati mwa viwanja vya Valiasr Square mjini Tehran kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Raisi na waziri wake wa mambo ya nje Hossein Amir-Abdollahian.
Shughuli za mazishi zitaanza leo katika eneo la Tabriz kwenye jimbo la mashariki mwa Azerbaijan kabla ya mwili wa Raisi kupelekwa Tehran na Khamenei anatarajiwa kuongoza swala ya kumuaga Raisi Jumanne jioni kabla ya msafara wa mazishi katika mji mkuu.



