MIRERANI, MANYARA
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amepongeza mchimbaji mdogo wa madini, Joseph Mwakipesile maarufu kama Chusa, kwa kutumia teknolojia na utaalamu wa kisasa katika shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa madini katika mgodi wake wa Chusa Mining, uliopo Mirerani.
Mavunde ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea mgodi huo na kujionea hatua mbalimbali za shughuli za uchimbaji, kuanzia utafiti, uchimbaji hadi uzalishaji wa madini ya Tanzanite.

Amesema Chusa Mining ni mfano wa mchimbaji mdogo anayepaswa kuigwa na wachimbaji wengine katika Mji wa Mirerani na ndani ya Eneo Tengefu la Mirerani, kutokana na namna kampuni hiyo inavyotumia mitambo ya kisasa pamoja na wataalamu katika shughuli zake.
Waziri Mavunde amewataka wachimbaji wengine wadogo kujifunza kutoka kwa Chusa Mining, hususan katika matumizi ya teknolojia, wataalamu wa jiolojia na upimaji wa miamba ili kuongeza ufanisi na uzalishaji.

Aidha, ameitaka kampuni ya Franone kuangalia kwa karibu namna wataalamu wa survey na geology wa Chusa Mining wanavyotekeleza majukumu yao kwa weledi, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia utaalamu na tafiti za kina katika kubaini maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuwa na madini.
Waziri Mavunde amesema utafiti wa kina ni jambo muhimu katika kuongeza uzalishaji wa madini nchini, akibainisha kuwa mabadiliko katika uzalishaji yanaweza kuchangiwa na kutokuwepo kwa tafiti za kutosha za kubaini maeneo na miamba yenye madini.

“Wachimbaji, hasa wachimbaji wadogo, lazima mjikite zaidi katika kufanya tafiti za uchimbaji. Utafiti wa kina ndiyo msingi wa kujua madini yako yapo wapi, kwa kiasi gani na namna bora ya kuyafikia,” amesema Mavunde.
Msisitizo huo unaendana na mikakati ya Wizara ya Madini ya kuimarisha utafiti wa madini na kuongeza uzalishaji, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa madini.

Kwa upande wake, Mmiliki wa Chusa Mining, Joseph Mwakipesile, alimweleza Waziri Mavunde namna kampuni yake inavyoendesha shughuli za uchimbaji wa Tanzanite, ikiwemo matumizi ya wataalamu na teknolojia katika hatua mbalimbali za uzalishaji.
Mwakipesile alisema alianza shughuli zake akiwa na mgodi mmoja, lakini kutokana na jitihada na uwekezaji katika sekta hiyo, kwa sasa anamiliki migodi minne inayofanya shughuli za uchimbaji.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya matokeo ya juhudi za kukuza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini, hususan kuwawezesha wachimbaji wadogo wazawa kukua kutoka shughuli ndogo za uchimbaji hadi kuwa wazalishaji wenye uwezo mkubwa zaidi.
Wizara ya Madini imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo na kuongeza matumizi ya teknolojia pamoja na tafiti za kisayansi ili kuongeza uzalishaji na manufaa ya rasilimali madini kwa Watanzania.

Chusa Mining sasa inaendelea kuonekana kama moja ya mifano ya mchimbaji mdogo mzawa anayelenga kutumia utaalamu, teknolojia na utafiti katika kuongeza uzalishaji wa Tanzanite, madini yanayopatikana kwa umaarufu mkubwa katika eneo la Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara.


