Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imewahukumu kunyongwa hadi kufa washtakiwa wawili kati ya wanne ambao ni Jumanne Kwangu na Daniel Kwangu, baada ya kupatikana na hatia ya mauji ya Kwalekwa Shiku na mtoto wake wa kiume Kuyonza Kubeja huku wengine wawili ambao ni Emanuel Kwangu na Mihayo Frednand wakiachiwa huru kutokana na ushahidi kutowatia hatiani.
Shauri hilo namba 128 la mwaka 2022 limesikilizwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Adrian Kilimi likiwahusu ndugu wa familia moja huku akisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka Mahakamni hapo umethibitisha pasipo kuacha shaka kwamba miongoni mwa washitakiwa wote wanne washitakiwa hao wawili wamethibitika kutenda kosa hilo.
Akisoma ushahidi mahakamni hapo jaji Kilimi amesema washitakiwa hao walitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti katika kipindi cha mwezi Mei 2019 ambapo walimshawishi Kuyonza Kubeja kwenda katika kijiji cha Katenka kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi ,kutafuta kazi na walipofika huko walimpleka chini ya Mlima Kasanga kisha kumuua kwa jembe na mwili wake kuuacha na wao kurejea katika kjiji cha Mwapanga Bure Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Aidha baada ya kurejea walimfata Kalekwa Shiku ambaye ni mama wa marehemu Kuyonza Kubeja na kumlaghai kuwa anaitwa kijiji jirani cha Mishepo na walipokuwa njiani walimuua kisha kumfunga kamba na kumuweka katika kiroba na kumtupa katika bwawa la maji mpaka pale mwili wake ulipoelea kisha kutambuliwa na ndugu zake, huku lengo la mauaji hayo ikielezwa kuwa ni kurithi mali ambazo ni mashamba na mifugo.
Shauri hilo kwa upande wa Jamuhuri limeongozwa na Wakili wa Serikali Reonald Kiwango na upande wa utetezi wakiongozwa na wakili Sulusi Mofati.