MATUMIZI TEKNOLOJIA YA UMWAGILIAJI KILIMI KUONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amefanya ziara ya kikazi katika Shamba la Mbegu Kilimi wilayani Nzega, mkoani Tabora, kukagua utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Oktoba 18, 2023.

Waziri Prof. Kabudi, aliyepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ametembelea bwawa la maji, karakana, nyumba za watumishi, eneo la kukaushia mbegu pamoja na mashamba ya uzalishaji wa mbegu.

Baada ya ukaguzi huo, Prof. Kabudi amepongeza Wizara ya Kilimo na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), kwa kusimamia mradi na kutekeleza maagizo ya Rais kwa ufanisi. 

Amesema hatua iliyofikiwa inaonesha thamani ya fedha zilizowekezwa na inaweka msingi wa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora nchini.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amesema matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji katika shamba hilo yatawezesha uzalishaji wa mbegu mwaka mzima badala ya kutegemea mvua za msimu huku akisisitiza kuwa hatua hiyo itaongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima, kuinua uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini. 

Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, ameomba Sekretarieti ya Mkoa kushirikishwa katika kamati za usimamizi wa mradi ili kuimarisha ufuatiliaji na kuwezesha changamoto kutatuliwa kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Tabora Upendo Wella amesema Mkoa wa Tabora unaendelea kuwa salama na kwamba ushirikiano kati ya Serikali Kuu na Mkoa utasaidia kuharakisha utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi hiyo ya maendeleo. 

Katika kikao cha majumuisho, Prof. Kabudi ametoa maelekezo 12, yakiwamo kutunza na kukarabati miundombinu na vifaa vya mradi, kukamilisha ujenzi wa ghala la kuhifadhia mbegu na kuweka mazingira ya kusimikwa kwa mtambo wa kuchakata mbegu.

Pia ameagiza mradi ukamilishwe kwa wakati, kwa viwango na ubora uliokusudiwa huku thamani ya fedha ikionekana wazi.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 11 umefikia asilimia 75 ya utekelezaji wa miundombinu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *