MATIBABU YA MACHO KUTOLEWA BURE SHINYANGA, WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA…

NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA 

WANANCHI wa Shinyanga, watakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kupata matibabu ya macho bure katika hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Macho wa Hospitali ya DrAgarwals tawi la Mwanza.

Wito huo umetolewa  na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu, Wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia maandalizi ya utoaji wa huduma hiyo ya macho bure kutoka kwa wadau hao wa Afya DrAgarwals Eye Hospitali.

Amesema utoaji wa huduma hiyo ya matibabu ya macho, utafanyika siku moja ya ijumaa ambayo itakuwa ni tarehe 10 januarI 2025 na kwamba wananchi wanapaswa kufika katika hospitali ya Manispaa kuanzia jumatano (Januari 08 2025)na Alhamisi kwa ajili ya kujiandikisha ili siku ya ijumaa iwe kwa ajili ya uchunguzi wa afya ya macho na kupata matibabu.

“Huduma hii ya matibabu bure ya macho itafanyika siku moja ya ijumaa, hivyo ni fursa kwa wananchi wa shinyanga wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa siku hizi mbili Jumatano na Alhamisi,ili waje kupata tiba, na hawa ni watalaamu wa macho na wanapandikiza hadi mboni ya jicho,” amesema Mlyutu.

“Tunampongeza sana Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya Afya, na leo hapa Shinyanga tumepata wadau wa Afya ambao wamekuja kuleta furaha kwa wananchi wa shinyanga,kwa kuwapatia huduma ya matibabu ya macho bure,”ameongeza Mlyutu.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga Dk.Pierina Mwaluko, amesema ujio huo wa madaktari wa macho hospitalini hapo, ni fursa kubwa kwa wananchi wa shinyanga katika kutatua matatizo yao ya macho.

Mratibu huduma za macho mkoani Shinyanga Dk.Joseph Edward, amesema tatizo la macho lipo mkoani humo, na kwamba kwa takwimu za miezi 10, iliyopita jumla ya  wananchi 14,624 walikuwa na tatizo la macho, huku 1,213 kati yao  walikuwa na mtoto wa jicho na walifanyiwa upasuaji.

Nao wadau hao wa Afya Gandhi Babu ambaye ni Mkuu wa Hospitali ya Macho ya DrAgarwals Tawi la Mwanza, amesema wameguswa kuja kutoa huduma ya matibabu ya macho kwa jamii bure, kutokana na wananchi wa Kanda ya Ziwa kukabiliwa na tatizo kubwa la macho.

Amesema katika huduma hiyo,watapima tatizo la uoni hafifu,presha ya macho,mtoto wa jicho, na kwamba wao ni wataalamu wa kupandikiza mboni ya jicho, na kuwasisitiza wananchi wa shinyanga wajitokeze kwa wingi kupata matibabu hayo siku hiyo ya ijumaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *