Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema
matarajio ya wananchi kwa Mahakama ya Tanzania ni kuona Mahakama hiyo inatenda
haki kwa wote na kwa wakati, akisisitiza uwajibikaji na ufanisi kama nguzo kuu katika
kuimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili huo.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo hii leo Juni 15, 2025 Ikulu Chamwino jijini Dodoma, katika hafla ya kumuapisha Jaji wa
Mahakama ya Rufani, George Mcheche Masaju kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika kuimarisha mifumo, miundombinu na mazingira ya utendaji kazi ili kuongeza ufanisi wa Mhimili huo wa dola.
Aidha, Rais Dkt. Samia pia ametoa msisitizo kwa Majaji wote kuendelea kusimamia misingi ya haki kwa uadilifu na weledi ili kuimarisha hadhi ya Mhimili huo duniani.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa Mahakama ya Tanzania
kuendeleza utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ili kuimarisha utawala wa
sheria na utawala bora nchini.
Rais pia qmemshukuru Jaji Mkuu Mstaafu, Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa mchango
mkubwa alioutoa katika kuongoza mageuzi ya miundombinu, mifumo ya kazi na ufanisi
wa utendaji ndani ya Mahakama ya Tanzania, akimtaja kama kiongozi aliyeacha alama ya
kudumu katika utumishi wake ndani ya Mahakama.

Jaji Mkuu Masaju amekuwa Jaji Mkuu wa kwanza kuapishwa jijini Dodoma tangu shughuli za Mahakama kuhamia rasmi Makao Makuu ya nchi.