Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa wiki sita huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka, ambayo yataanza kutekelezwa rasmi Jumapili ya Januari 19, 2025 yamepongezwa na Viongozi mbalimbali wa dunia.
Makubaliano hayo, yanajumuisha mambo matatu ya kumaliza vita hivyo ambapo jambo la kwanza ni kuwachiliwa kwa mateka 33 wa Israel, ambao wanashikiliwa na Hamas pamoja na wafungwa wa Kipalestina.

Viongozi hao akiwemo Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Wapalestina, Mohammed Mustafa wamesema makubaliano hayo yanatoa matumaini kwa raia wa pande zote na kwamba yatasaidia kuendeleza juhudi za kufanikisha amani ya kudumu, kati ya Israel na Palestina.
Wakati hayo yakijiri, inaarifiwa kuwa watu 12 wameuawa hii leo Januari 16, 2025 huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, baada ya Israel kushambulia kwa makombora jengo la makazi na kuzua sintofahamu.


