“Mashabiki wa Simba ni rafiki zangu”

Robertinho alisema bado timu hiyo inatakiwa kujengwa zaidi kufikia kwenye ubora ambao mashabiki wanautaka, kwa vile ina wachezaji wachache wenye viwango na waliosalia wanahitaji muda zaidi ya kujijenga kiasi hata mzunguko wa kubadilisha wachezaji ilikuwa ngumu kwake ingawa hakutaka kulalamika mbele ya mashabiki.

“Mashabiki wa Simba ni rafiki zangu watabaki kwenye moyo wangu wakati wote nitawakumbuka kila nilipokuwa nakutana nao viwanjani hata nikiwa matembezini walinipenda na nawapenda sana” alisema Robertinho na kuongeza;
“Lakini ni lazima waambiwe ukweli kwamba Simba ina safari ndefu kwa sasa kwa aina ya usajili uliofanyika na hata kwa wachezaji waliobaki kikosini, waliosajiliwa msimu huu ni Che Malone na Ngoma ndio wachezaji wenye ubora na viwango bora, wengine wanahitaji muda zaidi kuimarika.”

Alisema anaondoka Simba akiwa anajivunia rekodi nzuri aliyoiweka japo kipigo cha Yanga kimemtibulia, lakini anasisitiza amefurahia kuifundisha timu hiyo kongwe nchini na Afrika Mashariki.

“Safari yetu imeisha baada ya kupoteza mchezo mmoja tu, lakini nafurahi kuwaacha sehemu nzuri wakiwa juu ya msimamo na nimewapa heshima ya kuwa na taji, wanatakiwa kujua ukweli kwamba Simba ina timu nzuri lakini bado inahitaji kujengwa zaidi.
“Hakuna njia ya mkato kwenye kutafuta mafanikio kupata timu bora huwezi kuijenga kwa kutumia dirisha moja la usajili, ukiangalia safari ni hao wawili walioingia kikosi cha kwanza, waliosalia wanajitafuta. Jambo zuri Simba itajivunia tulibakiza wachezaji waliokuwa msingi wa timu ambao walipounganika na wengine tukajaribu kuwa na timu yenye upinzani.”
Robertinho alisema kwa sasa anarudi kwao Brazil kupumzika kwa muda na familia yake kabla ya kutafuta akili mpya ya maisha yake, huku akiweka bayana kwamba licha ya Simba kupoteza mechi moja bado ina nafasi ya kushindania ubingwa, kwa vile kuna mechi nyingi mbele kabla ya msimu kumalizika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *