Imeandikwa na Ibrahim Rojala,kwa Msaada wa Mtandao
Marekani imesisitiza pande zinazohasimiana Israel na Hamas juu ya umuhimu wa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa takriban miezi 11 katika Ukanda wa Gaza na kuwaachia huru mateka waliosalia ambao wako mikononi mwa Hamas.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje ya Marekani Mathew Miller amewaambia hayo waandishi wa habari baada ya vikosi vya Israel kupata miili ya mateka sita mwishoni mwa juma waliokuwa chini Hamas katika handaki lililopo Rafah kusini mwa Gaza.
Miller amesema Marekani itafanya kazi katika siku zijazo na wapatanishi Misri na Qatar kuongeza kasi ya makubaliano ya mwisho na kudokeza kwamba Jambo moja kuu la mzozo katika mazungumzo hayo ni kusisitiza kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwamba wanajeshi wa Israel, wabaki kwenye mpaka kati ya Gaza na Misri.
Aidha mpaka sasa bado kuna mateka kadhaa wanaoendelea kushikiliwa Gaza katika kipindi ambacho bado wanasubiri makubaliano ambayo yatawawezesha kuachiliwa huru na kurejea nyumbani.
Wakati huo huo, Wizara ya Sheria ya Marekani imetangaza mashtaka ya jinai dhidi ya kiongozi wa Hamas, Yahya Sinwar na wanamgambo wengine wakihusishwa na shambulizi la Oktoba 7, 2023 nchini Israel.
Mashitaka ya jinai yaliyowasilishwa katika mahakama ya serikali kuu jijini New York yanajumuisha mashtaka ya kula njama ya kutoa msaada wa mali kwa shirika la kigeni la kigaidi, na kusababisha vifo.