MAPUNG’O FOUNDATION WAKABIDHI MAGUNIA 75 YA MAHINDI NYAKAGWE SEKONDARI GEITA

Na Ibrahim Rojala – Geita.

Taasisi ya Mapung’o Foundation ya Mkoani Geita imetoa msaada wa Magunia 75 ya Mahindi na bunda za karatasi boksi 17, katika Shule ya Sekondari Nyakagwe iliyopo Kata ya Butobela halmashauri ya wilaya ya Geita Mkoani Geita.

Mratibu wa Taasisi hiyo,Marko Victor amesema kuwa msaada huo umetolewa lengo la kupunguza changamoto ya upatikanaji wa chakula na karatasi hizo kwa wanafunzi wanaotoka katika familia zenye changamoto za kiuchumi katika shule hiyo na kueleza kwamba Tasisi hiyo itaendelea kusaidia jamii katika sekta mbalimbali kwa kadri itakavyowezekana.

“Hii ni miongoni mwa projects zetu ambazo tuko nazo,taasisi yetu imekuwa ikijihusisha na kusaidia Jamii,kadri ya uwezekano tutakuwa tukifanya,sio tu upande wa elimu bali kwa uhitaji wowote tutakuwa tukisaidia”amesema Marko

Akizungumza Mara baada ya kupokea msaada huo,Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyakagwe yenye jumla ya wanafunzi 452,George Edward ameeleza kuwa msaada huo utakuwa chachu ya uwezeshaji wa upatikanaji wa chakula shuleni kwa wanafunzi kutokana na uwepo wa changamoto ya baadhi ya wazazi kusua sua katika uchangiaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni husuani kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne walio katika Programu maalum za masomo katika shule hiyo.

“Kupitia huu msaada na wazazi wengine watakaochangia kwaajili ya zoezi la chakula, wanafunzi watakuwa na muda mwingi  wa kujisomea wanapokuwa shuleni kwasababu tuna Programu ya madarasa yote,”

“Tunavyomaliza vipindi muda wa kawaida wanaenda kula,lakini wanafunzi wa kidato cha nne na kidato cha pili wao wanaendelea kubaki shuleni kwasababu kuanzia saa moja tuna ratiba ya vipindi pia mpaka saa mbili usiku,” ameeleza Mwalimu George.

Mwanafunzi, Nelson Joseph wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Nyakagwe ameeleza kuwa imekuwa furaha kubwa kwa wanafunzi kupata msaada huo na kuishukurua Taasisi ya Mapung’o Foundation akieleza kwamba hawatopoteza tena muda kufuata chakula nyumbani katika kipindi ambacho walipaswa kuendelea na masomo na kuiomba taasisi hiyo pia kuwasaidia kupata baadhi ya vifaa vya maabara hatua itakayowawezesha kujifunza kwa ufanisi zaidi.

“Tunaomba kwa hali hii mnavyoendela kutusaidia  kwa moyo mlio nao wa  kutuona kwamba na sisi tunafaa, mzidi kuwa nayo na kwa vitu vingine ambavyo tunapelea mfano maabara kuna wanafunzi wanasoma  sayansi, kuna vifaa vya maabara ambavyo havipo,”

“Kuna test ambazo zilitakiwa kufanywa labda na wanafunzi ambao wanafanya sasa hivi mtihani practical lakini tuna uhaba wa vifaa hivyo ningependa wangezidi tu kutusaidia kwa hivyo vitu ili tuweze kuongeza Perfomance katika masomo,” amebainisha Nelson.

Naye Lucy John Renatus, mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo ameeleza kwamba msaada wa bunda za karatasi umesaidia kuwaondolea changamoto wanafunzi wapatao 84 ambao walikuwa hawajatoa mchango huo.

Amessma, kwa upande wa mahindi yatawasaidia kupata muda mrefu wa kujisomea wakiwa shuleni hususani katika muda wa jioni kwakuwa ilikuwa ni vigumu kwa wanafunzi kuendelea na masomo wakiwa hawajapata chakula katika nyakati hizo.

Afisa Elimu kata ya Butobela,Ndio John Otieno ameishukuru Taasisi ya Mapung’o Foundation kwa namna ambavyo imeendelea kutoa msaada katika sekta ya elimu ndani ya kata hiyo akieleza kwamba imekuwa ikigusa kila mwananchi kupitia elimu na kuikaribisha katika shule zingine zenye mahitaji mbalimbali na kutumia fursa hiyo kuzikaribibisha taasisi mbalimbali katika shule zilizopo ndni ya kata hiyo.

Ameuelezea msaada huo kuwa utachochea ukuaji wa elimu kwa wanafunzi wa jinsi zote katika shule ya Sekondari Nyakagwe, kurahisisha na kuleta ufanisi katika elimu kwa wanafunzi wa kike walio na hosteli katika shule hiyo na wavulana wanaotarajia kuweka kambi.

Kambi hiyo ilihitaji gharama za uendshaji ikiwemo chakula, eneo ambalo Taasisi ya Mapung’o Foundation imetatua changamoto iliyokuwepo na kueleza kwamba ni matarajio ya serikali kuona chakula hicho kikisaidia kuwezesha wanafunzi kukaa kwa utulivu kusoma vizuri na kuborsha taaluma na matokeo kwa ujumla.

Taasisi ya Mapung’o Foundation ilianzishwa mwaka 2023 na kusajiliwa rasmi mwaka 2026 ikijihusisha na kutatua changamoto mbalimbali ndani ya Jamii inayofanyia kazi kwa kuboresha mazingira na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa jamii husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *