MAONESHO YA NANENANE IPULI YAENDELEA KUWANUFAISHA WANANCHI TABORA

Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wajasiriamali wameendelea kunufaika na Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Magharibi baada ya kushiriki kongamano maalum lililofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Fatma Mwasa, Ipuli, Manispaa ya Tabora.

Kongamano hilo, linalenga kuwajengea maarifa na ujuzi wa kuongeza tija, ubora wa uzalishaji na upatikanaji wa masoko. Katika kongamano hilo, wataalamu kutoka taasisi mbalimbali wamewasilisha mada zinazogusa moja kwa moja shughuli za uzalishaji na biashara.

Kassim Majiji kutoka Wakala wa Vipimo ametoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo katika biashara, huku Gabriel Ngogo kutoka TARI Tumbi akieleza kuhusu mbinu za kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi ili kuwawezesha wakulima kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri uzalishaji.

Kwa upande wa pembejeo na masoko, Evance Kaganda kutoka TOSCI ametoa elimu kuhusu utambuzi wa mbegu bora pamoja na namna ya kutumia vigezo vya ubora, huku Mary Mlay kutoka COPRA akielezea mfumo wa masoko ya minada ya kidijitali na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo. 

Aidha, Andishile Mwakalobo kutoka TMX amewajengea washiriki uelewa kuhusu masoko ya kidijitali na matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani katika kuwawezesha wazalishaji kupata fursa bora za masoko. 

Katika kuongeza uwezo wa wakulima kufanya kilimo cha kibiashara, Meneja Mahusiano Kanda ya Magharibi wa Idara ya Kilimo NMB, Samwel Mwandalima, ameeleza fursa mbalimbali za huduma za kifedha zinazolenga sekta ya kilimo, zikiwemo mikopo ya pembejeo, uwezeshaji wa kilimo cha kibiashara pamoja na huduma za bima zinazosaidia kupunguza vihatarishi katika shughuli za uzalishaji.

Naye Kaimu Meneja wa Kampasi ya FETA Kigoma, August Damian Shirima, amewasilisha mada kuhusu ufugaji wa samaki, uzalishaji wa funza kwa ajili ya chakula cha mifugo pamoja na fursa za mafunzo zinazopatikana katika Kampasi ya FETA Kigoma.

Sekta za mifugo na uvuvi pia zimepewa nafasi katika kongamano hilo ambapo Denis Luwumba kutoka TVLA ametoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya chanjo na uchunguzi wa magonjwa ya mifugo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *