Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Thomas Myinga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ameongoza Kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa wa Tabora kilichofanyika katika Ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi, mjini Tabora.
DC Myinga amezitaka mamlaka zinazosimamia biashara kuzingatia sera, sheria na kanuni ili kuondoa kero, kupunguza urasimu na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji.

Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wa Serikali, sekta binafsi na wadau wa uwekezaji kujadili changamoto za biashara, taarifa za mabaraza ya wilaya na mikakati ya kuvutia uwekezaji mkoani Tabora.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Upendo Joseph Haule, amezitaka halmashauri kukamilisha maandiko ya miradi ya uwekezaji na kuyawasilisha Ofisi ya Rais–TAMISEMI pamoja na Kitengo cha PPP.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, amezitaka taasisi za fedha kuongeza elimu kuhusu vigezo na masharti ya mikopo.
Mwenyekiti wa TNCC Mkoa wa Tabora, Kitwana Kasongo, amesema mabaraza hayo yanawapa wafanyabiashara fursa ya kuwasilisha changamoto zao kwa Serikali na kushiriki katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu.






