MAMIA WAFURIKA MPIMBWE KUPATA HUDUMA ZA NIDA, WATOA OMBI KWA SERIKALI

Na Daniel Gahu – Katavi.

Wananchi wa Kata ya Majimoto katika Halmashauri ya Mpimbwe, mkoani Katavi, wameiomba Serikali kusogeza huduma za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) karibu na maeneo yao, wakieleza kuwa umbali wa kufuata vitambulisho hivyo unawawia vigumu kupata huduma mbalimbali zinazohitaji kitambulisho cha taifa.

Wananchi hao wamesema ukosefu wa huduma hizo katika maeneo yao unawalazimu kusafiri umbali mrefu kufuata vitambulisho, hali inayowaongezea gharama na muda wa kufuata huduma hiyo muhimu.

Wakizungumza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wananchi, baadhi yao wamesema kutokuwa na vitambulisho vya taifa kumekuwa kikwazo katika kupata huduma mbalimbali zinazohitaji kitambulisho hicho.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa NIDA Wilaya ya Mlele, Frank Mrutu, amesema NIDA inaendelea na juhudi za kuwafikia wananchi katika maeneo yao, ikiwemo kuanzisha kliniki tembezi zitakazosaidia kusogeza huduma karibu na wananchi.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kujiandikisha na kupata huduma za NIDA bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Wakati huohuo, kuelekea maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Halmashauri ya Mpimbwe, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kalokola Kasimbazi, amesema maadhimisho hayo yatatumika kama fursa ya kusogeza huduma mbalimbali karibu na wananchi.

Kasimbazi amesema pia maadhimisho hayo yatatumika kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kubaini mafanikio na changamoto zilizopo, pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema tathmini hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma na maendeleo ya Halmashauri hiyo sambamba na kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Wananchi sasa wanatarajia hatua zaidi kutoka kwa Serikali na NIDA katika kuhakikisha huduma za vitambulisho vya taifa zinawafikia kwa urahisi, hususan wananchi wa maeneo ya vijijini ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya umbali na gharama za usafiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *