Mama Lishe Walizwa na Mdororo wa Biashara Majengo,Kahama

Wajasiriamali wanawake wanaojihusisha na biashara ya chakula maarufu kama mama Lishe wanaofanya shughuli zao katika jengo lililopo kata ya Majengo Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga wamelalamikia kukosekana kwa wateja katika eneo hilo hali inayowasabishia maisha magumu wao na familia zao kutokana na mdororo wa biashara uliopo katika hivi sasa.

Wakizungumza na Jambo Fm   hii Leo Mei 6,2024 Mama Lishe hao wamesema kuwa hali ya biashara imekuwa ngumu baada ya mabasi yaliyokuwa yakipakia abiria katika eneo hilo kuhamishwa kutoka katika njia lililopo jengo hilo linaloelezwa kuwa lipo katika eneo ambalo si rahisi kuonekana kwa wateja.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao Jackline Anatory ameiomba serikali kuondoa vibanda vilivyopo mbele ya jengo husika ili liweze kuonekana pamoja na kurejesha huduma ya mabasi yaliyokuwa yanafanya kazi katika eneo hilo ili waweze kufanya biashara, pia wakiomba kuimarishiwa ulinzi.

Diwani wa kata ya Majengo Bernard Mahongo amekiri uwepo wa changamoto hiyo na kueleza kwamba hali hiyo imetokana na kupungua kwa magari na kubainisha kuwa muda wowote kuanzia sasa magari yaliyokuwa yakifanya kazi katika kituo hicho yatarejeshwa na kutoa wito kwa wafanyabiashara kuwa na subira hadi pale huduma ya mabasi itakaporejea.

Jengo hilo lililopo kata ya Majengo Manispaa ya Kahama lenye vyumba 12 lililogharimu kiasi cha shilingi milioni 183 lilifunguliwa rasmi mwaka 2018 kupitia mbio za mwenge wa uhuru.

One response to “Mama Lishe Walizwa na Mdororo wa Biashara Majengo,Kahama”

  1. Kiukweli Hata serikali ione aibu,,unawezaje kujenga jengo kubwa namna hiyo pia kwa mamilioni alafu usiweze kuangalia njia nzuri ya kuweza kujipatia mapato bana.tutafurahi sana kama watarejeshewa huduma hiyo mama lishe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *