Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC limesema kuanzia Oktoba 2 2023 litaanza kuwatoza faini wamiliki wa Mabasi, Malori yanayofanya safari ndani na nje ya nchi na magari mengine binafsi ambayo yanasimama porini ili kuruhusu abiria kujisaidia maarufu “kuchimba dawa”.

Mkurugenzi mkuu wa NEMC Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka amesema kabla ya kuanza kutoza faini kwa mabasi na magari yanayosimama porini ili abiria kutojisaidia watatoa elimu kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Septemba 2 hadi Oktoba 2 na kueleza kuwa umefika wakati sasa magari ya abiria yaendayo mikoani yawe na vyoo ndani ili kuwasitiri abiria pamoja na kutunza mazingira.
Dokta Gwamaka amezitaja adhabu za kisheria kwa mabasi ya abiria na magari mengine ni pamoja na kutozwa faini isiyopungua shilingi milioni 5, kufutiwa leseni ya usafirishaji abiria au zote kwa pamoja na pia watashirikiana na halmashauri za maeneo husika kuhakikisha vyoo vinajengwa kila baada ya umbali kadhaa ili kusaidia kutunza mazingira.
Aidha katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa NEMC itatoa motisha ya fedha kwa atakayefanikiwa kupiga picha ikionesha namba ya gari na ushahidi wa watu ambao wakiwa katika eneo hilo la kujisaidia.