Na Gideon Gregory – Dodoma.
Serikali imesema imekamilisha hatua muhimu za kisheria za kuwatambua maveterani walioshiriki katika Vita vya Kagera dhidi ya utawala wa Idi Amin wa Uganda, na sasa inalenga kuanza kuwalipa ndani ya mwaka huu wa fedha.
Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 3,2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la Mbunge Nkasi Kaskazini Bazilio Mbwilo, aliyehoji ni lini serikali itaanza rasmi kuwalipa maveterani hao ambao wamekuwa wakisubiri malipo kwa miaka mingi.

Waziri Mkuu amesema kuchelewa kwa malipo hayo kulitokana kwa sehemu na changamoto za kisheria, ambapo baadhi ya wapiganaji walioshiriki katika vita hivyo hawakuwa wanatambuliwa chini ya sheria zilizokuwepo wakati huo.
“Serikali tayari imefanya marekebisho ya sheria ili kuwatambua maveterani hao, huku hatua iliyobaki ikiwa ni kukamilisha taratibu za malipo kwa kushirikisha Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,”amesema.

Ameeleza kuwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa jambo hilo zimezingatiwa katika bajeti, na kwamba baada ya kukamilishwa kwa taratibu za malipo, malipo yataanza ndani ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Waziri Mkuu pia amezielekeza Wizara ya Fedha na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kukaa pamoja na kuharakisha mchakato huo ili maveterani hao, ambao walishiriki katika vita vya mwaka 1978 na 1979, waanze kupata stahiki zao.


