
Na Adam Msafiri, Musoma Mara.
Imeelezwa kuwa ni malengo ya serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha mpaka kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi kote nchini wawe wanatumia nishati safi na salama ya kupikia majumbani mwao.
Akiwa katika hafla fupi ya kukabidhi majiko ya nishati safi ya kupikia kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza mkoa wa Mara Julai 2,2025, Bw.Lucas Malunde ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya nishati safi vijijini (REA) amesema Wakala wa nishati vijiji(REA) utahakikisha unafikia malengo hayo kabla ya mwaka 2034 na hii ni kutokana na mikakati waliyojiwekea.

“Ni malengo yetu kwamba kama mkakati unavyosema inapofikia mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia na kwa kweli sisi ndani ya Rea sio yu tunasubiri mwaka 20234,tunatamani sana hata kabla ya mwaka 20234 tuwe tumeshalifikia lengo hilo”. Amesema Bw.Malunde.
Aidha mjumbe huyo wa Bodi ya Wakala wa nishati vijijini(REB) amelitaka jeshi la Magereza nchini kuwa balozi mzuri wa kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya nishati safi huku akilipongeza Jeshi hilo kwa kuendelea kutekeleza maelekezo ya serikali ya kuachana mara moja na matumizi ya kuni na mkaa kama nishati ya kupikia,kwani nishati hiyo si salama kwa afya ya binadamu na inahatarisha mazingira.
Naye Dkt. Joseph Sambali ambaye ni Mtaalamu wa nishati na Jinsia kutoka Wakala wa nishati vijijini(REA)amesema”Ruzuku ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni 35 imetolewa na serikali ili kuhakikisha magereza yote nchini yanatumia nishati safi ya kupikia, ambapo pamoja na mambo mengine fedha hizo zitatumika kuweka miundombinu ya nishati safi magerezani”.Ameeleza Dkt Sambali.
Dkt Sambali amebainisha kuwa kupitia mradi huo wa usambazaji wa majiko ya nishati safi,inatarajiwa zaidi ya mitungi ya gesi elfu 15 itatolewa kwa watumishi na askari wote wa Jeshi la Magereza mkoani Mara.

Akitoa taarifa kuhusu hatua zilizochokuliwa na Magereza mkoani Mara,Mkuu wa Magereza katika mkoa huo Kamishna Msaidizi wa Magereza Hospcious Mendi amesmea kuwa tangu Desemba 31,2024 magereza yote mkoani Mara yalihama kutoka kutumia nishati ya kuni na mkaa katika mapishi na kujielekeza kwenye matumizi ya nishati safi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa hara ya maagizo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Aidha mradi wa usambazaji wa majiko ya nishati safi sit u unalenga taasisi za umma bali pia ni dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wa kawaida wanapata majiko ya gesi kwa bei nafuu hali itakayosaidia kuihamasisha jamii kuachana na matumizi ya nishati chafu hali itakayowezesha kuokoa maisha ya wengi pamoja na kulinda mazingira.