Na Gideon Gregory – Dodoma.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Serikali kutoa ruzuku kwenye bei ya mafuta, ili kupunguza makali ya gharama hiyo muhimu kwa wananchi.
Akizungumza leo Aprili 7, 2026 Jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari kuhusu mfumuko wa bei ya mafuta, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amesema kupanda kwa bei ya mafuta ni changamoto ya kimataifa na si suala la kisiasa.
Kihongosi amesema kuwa CCM, kupitia Serikali yake, imeanza kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzisha Mfuko wa Kuhimili Ukali wa Bei za Mafuta, ambao uko katika hatua za mwisho za maandalizi. Mfuko huo unalenga kupunguza makali ya bei za mafuta pale zinapopanda kwa kiwango kikubwa.

“Serikali inaendelea na mpango wa kuanzisha hifadhi ya mafuta ya kimkakati ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unakuwa wa uhakika hata wakati wa changamoto. Sambamba na hilo, ujenzi wa maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta unaendelea, hatua itakayosaidia nchi kupata mafuta kwa bei nafuu na kuimarisha biashara ya nishati,” amesema Kihongosi.
Aidha, maboresho yanafanyika katika mfumo wa uagizaji wa mafuta kupitia ghala moja (Single Receiving Terminal – SRT) ili kupunguza gharama zisizo za lazima, ikiwemo zile zinazohusiana na meli kusubiri kupakua mafuta. Hatua hii inalenga kuongeza uwazi na ufanisi katika sekta ya mafuta.
Vilevile, Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) limeongezewa uwezo wa kuagiza mafuta moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji bila kupitia madalali, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama na bei kwa mtumiaji wa mwisho. Taasisi nyingine kama EWURA na PBPA nazo zinaimarishwa ili kuhakikisha ununuzi wa mafuta unafanyika kwa gharama nafuu zaidi.
Kihongosi amesema kuwa katika mkakati wa muda mrefu, CCM imeweka mkazo katika kuwekeza kwenye nishati mbadala na usafiri wa umma wa kisasa, ikiwemo matumizi ya gesi asilia (CNG) na magari ya umeme. Hatua hii inalenga kupunguza utegemezi wa mafuta, gharama za usafiri na matumizi ya fedha za kigeni.
“CCM imesisitiza umuhimu wa kujenga uchumi wa uzalishaji unaolenga kuuza nje, pamoja na kupitia upya tozo na kodi kwenye mafuta ili kupunguza gharama kwa wananchi. Licha ya changamoto hii kuwa ya kimataifa, tuna imani kuwa chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, nchi itaweza kuvuka kipindi hiki na kujenga uchumi imara zaidi,” amesema Kihongosi.
Ameongeza kuwa CCM itaendelea kuisimamia Serikali kwa karibu ili kuhakikisha hatua zote zinazochukuliwa zinalenga kulinda maslahi ya wananchi na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
Hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za maisha kwa wananchi, hasa katika kipindi hiki ambacho bei ya mafuta imekuwa ikipanda na kuathiri sekta mbalimbali za uchumi.