
Na Gideon Gregory, Dodoma
Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Esther Matiko, ameishinikiza Serikali kuhakikisha kuwa wingi wa makabila yaliyopo nchini unatumiwa ipasavyo kuvutia watalii kupitia tamaduni zao, kama inavyofanyika kwa jamii ya Wamasai.
Mhe. Matiko ametoa wito kwa Serikali kuweka mpango madhubuti wa kujenga kituo maalum kitakachotumika kutangaza na kuhifadhi tamaduni mbalimbali za zaidi ya makabila 120 yaliyopo nchini, ili kuendeleza utalii wa kiutamaduni na kuongeza pato la taifa.
Akijibu hoja hiyo leo Mei 14,2025 Bungeni, Jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, amekiri kuwa kwa wingi wa makabila nchini, yapo mambo mengi yanayoweza kutumika kama vivutio vya utalii. Aidha, alieleza kuwa Wizara ina mikakati ya kuanzisha aina mpya za utalii zitakazojumuisha mila, tamaduni, na vyakula vya asili.
“Hivi karibuni tumefanya kongamano kubwa la utalii wa vyakula hapa nchini. Tunayo mipango ya kutekeleza mambo haya ambayo Mbunge amependekeza, tunaomba muda ili tuyakamilishe,” amesema Kitandula.