Zaidi ya wananchi 10,000 katika kata Busangi halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamenufaika na mradi wa maji wa Ziwa Victoria wa Nduku Busangi wenye thamani wa shilingi bilioni 5.31 unaotekelezwa na RUWASA Kahama kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani kwa kuondoa changamoto ya kukosekana kwa maji ambayo ilikuwa ni ya muda mrefu.
Wakizungumza mbele ya mkuu wa wilaya ya Kahama wakati wa akikagua mradi huo pamoja na kuuzindua ili uanze kufanya kazi, Bi.Maria Cosmas na Bw.Shija Mihayo wameishukuru serikali kwa kuwatatulia changamoto ya ukosefu wa maji, ambapo awali walikua wakitembea umbali mrefu hali ambayo wakati mwngine ilisababisha kuvunjika kwa ndoa zao.
Baada ya ukaguzi na uzinduzi,mkuu wa wilaya ya Kahama Bi.MboniMhita amesema kuwa Mtandao wa maji uliojengwa kupitia mradi huo utasambazwa ili kuzinufaisha takribani kata tano za halmashauri hiyo na kuwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji ambayo imeweza kutatua changamoto ya wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Kwa upande wake meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijiji (RUWASA) wilaya ya kahama Mhandisi Maduhu Mahili amesema usambaji wa mabomba ya chuma yenye urefu wa kilometa 18.92 umekamilika na maji yamefika katika vijiji vya Busangi na Nyamigege kwa gharama ya shilingi bilioni 2.98, huku mradi ukiwa umekamilika kwa asilimia 85% na mpaka sasa kiasi cha shilingi bilioni 3.66 zimetumika katika utekelezaji wa Mradi huo.