MAJI YA ZIWA VICTORIA KUWAFIKIA WANANCHI BUSANDA

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, ameendelea na ziara yake katika hilo na sasa amewapa matumaini wananchi wa Kijiji cha Singita katika Kata ya Usanda, baada ya kutangaza kutatuliwa kwa changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama, kufuatia  kuanza kwa mchakato wa kusogeza maji ya ziwa Victoria kutoka Tangi la Buchama.

Azza ametoa kauli hiyo, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Kijiji cha Singita kilichopo katika kata hiyo ya Busanda.

Amesema, hatua hiyo imefikiwa baada ya kikao alichofanya na Waziri wa Maji Jumaa Aweso, pamoja na wataalamu wa wizara hiyo, ambapo aliambiwa  na Rais Dk. Samia Suiluhu Hassan kwamba haiwezekani Tangi la Maji lipo Buchama harafu wananchi wanaozunguka Tangi hilo wakose maji, huvyo serikali imehakikisha wananchi wanaozunguka miundombinu ya maji wanapata huduma ya nishati hiyo.

“Ninafuraha kuwaambia kuwa kikao kile kimeleta majibu. Wameshakuja watu wa RUWASA na wamefanya tathmini yote, na muda wowote ndani ya mwaka huu wa fedha 2026/2027 maji yatatoka Buchama na kuletwa Usanda Singita,” amesema Azza.

Amesema jukumu lake kwa sasa ni kuendelea kufuatilia utekelezaji wa mradi huo ili uanze kwa haraka, huku akieleza kuwa baada ya maji kufika Usanda, yataendelezwa kwa matawi yatakayofikisha huduma hiyo katika maeneo ya Ngaganulwa, Shabuluba na Nzagaluba.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ameeleza kuwa Serikali imetenga Sh milioni 137.9 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la barabara ya Usanda–Masunula, ambapo taratibu za kumpata mkandarasi zinaendelea.

Amesema ujenzi huo unatarajiwa kuanza baada ya taratibu kukamilika, huku akibainisha kuwa ndani ya kipindi cha miezi sita wananchi wanatarajia kuona utekelezaji wa mradi huo.

Kuhusu huduma ya umeme, Azza amesema vitongoji vya Manyinya na Matanda vilivyopo Singita tayari vimefanyiwa usanifu na vipo katika hatua za kuendelea na utekelezaji wa mradi huo.

Wananchi wa Singita walitumia mkutano huo kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara, kutokamilika kwa ujenzi wa zahanati pamoja na ukosefu wa maji safi na salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *