MAJALIWA ACHAGIZA SIKU YA TANZANIA MAONESHO YA EXPO 2025, JAPAN

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara kati ya Tanzania na Japan kutoka dola za kimarekani bilioni 7 mwaka 2020, hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 37 mwaka 2024 na hivyo kukuza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye nyanja za kiuchumi.

Majaliwa ameyasema hayo leo Mei 25, 2025 jijini Osaka Japan wakati akimwakilisha Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye maadhimisho ya Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya Osaka Expo 2025 yanayoendelea nchini Japan,ambapo amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji kwenye miradi ya Jotoardhi, Uchumi wa buluu, Afya, Elimu, Miundombinu, Kilimo, na Mifugo.

Aidha Majaliwa ametumia fursa ya siku ya Tanzania kuyaalika kampuni za Japan kuwekeza nchini pamoja na kushiriki kwenye maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama sabasaba ambayo hufanyika kuanzia mwishoni mwa mwezi juni.

‘’Nipende kuwakaribisha wenzetu wa Japan kuja kuwekeza Tanzania kwani mazingira ya uwekezaji ni mazuri,‘’ amesema Majaliwa.

Siku ya Tanzania kwenye maonesho ya Osaka Expo 2025 nchini Japan ilipambwa na ngoma za utamaduni na Taarabu asilia kutoka Zanzibar na kuhudhuriwa pia na Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa taasisi mbalimbali sambamba na maonesho ya Wiki ya Miundombinu ya Osaka Expo 2025 yanayoendelea nchini Japan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *