Na Eunice Kanumba- Shinyanga.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Shinyanga, limekabidhiwa magari matano na serikali ambayo yataongeza ufanisi wa utendaji katika kukabiliana na majanga mbalimbali ya uokoaji watu na mali zao.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amekabidhi Magari hayo mbele ya viongozi wa jeshi hilo, huku akieleza kuwa magari hayo yakatumike kama ilivyokusudiwa.

Ametumia jukwaa hilo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuyajali Majeshi akisema yataongeza chachu ya utendaji kazi.
“Katika Mkoa wa Shinyanga tumepewa Magari Saba,lakini leo nakabidhi Magari Matano ambayo ndiyo yamefika,gari moja nila kuzimia moto,mawili ya kubeba majeruhi,Jingine la kufanya mawasiliano (Control Unit) na la kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kukabiliana na majanga,” amesema RC Mboni.

Aidha, amaetoa wito kwa Wananchi kuwa kwenye shughuli zao za ujenzi na uwekezaji wa miundombinu walishirikishe Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ili wapate ushauri na kupunguza athari za majanga.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Shinyanga, Thomas Majuto amesema Magari hayo yanakwenda kuongeza ufanisi mkubwa wa utendaji kazi na hata kufika kwa haraka kwenye majanga na kufanya maokozi.

Majuto ameongeza kuwa, kwa mkoa mzima wa Shinyanga walikuwa na Magari Mawili tu ya kuzimia Moto lakini sasa hivi yamefika Matatu,pamoja na kupata Magari ya kubeba Majeruhi ambayo hawakuwa nayo kabisa.


