Na Daniel Gahu – Katavi.
Baada ya mvua kubwa kunyesha wiki iliyopita na kusababisha kaya kadhaa kuathirika katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, wakazi wa Kijiji cha Ikola wamepatiwa mafunzo ya matumizi bora ya ardhi.
Mafunzo hayo, yameendeshwa na Halmashauri ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu, aliyesisitiza kuondolewa sintofahamu katika ugawaji wa maeneo.

Katika mafunzo hayo, Afisa Maendeleo ya Ardhi wa Wilaya, Elisha Mengele ameeleza kuwa ili kuondoa migogoro ya ardhi hususani katika Kijiji cha Ikola, ni muhimu kufanyika upimaji jumuishi wa maeneo ya vijiji.
Kupitia zoezi hilo, kila kaya iliyoathirika na mvua kubwa itapatiwa eneo maalum, huku maeneo mengine yakitengwa kwa matumizi ya kijamii na ya kibinadamu ili kuondokana na athari za janga la mafuriko ambalo limekuwa likisababisha hasara kwa wananchi kwa kuharibikiwa na Mali zao.

Aidha, wananchi wa Ikola wameiomba ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuendesha zoezi la kuonesha mipaka ya viwanja vilivyopimwa, ili kugawa viwanja hivyo kwa waathirika wa mvua. Ombi hilo limepokelewa rasmi na utekelezaji wake umeanza mara moja ili kuhakikisha kaya husika zinahamishiwa katika maeneo salama.
Hatua hii inalenga kulinda wakazi dhidi ya athari za mvua kubwa na kuimarisha matumizi bora ya ardhi kwa manufaa ya jamii.

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, imesisitiza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu, likihusisha ushirikiano wa wananchi, viongozi wa mitaa na wataalamu wa ardhi, ili kuhakikisha kila kaya inapata haki na usalama wa makazi.

