Madiwani walalamikia mfumo wa Matibabu Hospitali ya Wilaya Kahama

Baraza la madiwani manispaa ya Kahama limelalamikia kitendo cha kususuasua kwa mfumo wa matibabu katika hospitali ya manispaa ya Kahama hali inayosababisha wagonjwa kuchelewa kupata matibabu kwa wakati.

Hayo yamesemwa na baadhi ya madiwani wa manispaa ya Kahama wakati wakichangia hoja kwenye kamati ya afya na elimu katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika manispaa hiyo.

“Katika hopsitali yetu ya manispaa ya kahama kumekuwa kuna shida sana ya mfumo katika matibabu, mgonjwa anapokwenda kutibiwa unaambiwa mfumo hakuna,mfumo mbovu anakaa kusubiri hadi mfumo utakapokamilika”.

Awali akitoa majibu kuhusu kususua kwa mfumo huo Mganga Mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Kahama Baraka Msumi amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba huwa wanamtumia mtaalamu wa Tehama kurekebisha tatizo linapotokea huku akisema kuwa inaposhindikana wanaendelea na matibabu bila kutumia mfumo.

“Ni kweli huwa tunapata changamoto za mfumo lakini tunachokifanya huwa tunawasiliana na mwezetu wa tehama na akibaini changamoto ni kubwa huwa tunaendelea nq matibabu nje ya mfumo”

Kwa upande wake mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Masood Kibetu amesema kuwa changamoto ya mfumo isiwe kigezo kwa wananchi kutopatiwa matibabu na kwamba kwasasa wameweka mfumo wa kuwahudumia wagonjwa hata kama mfumo umeleta shida.

“Kama mfumo haufanyi kazi isiwe kigezo cha wagonjwa kutotibiwa,kwa pale hospitali wagonjwa wote watatibiwa mfumo ukiwa unafanya kazi au haufanyi kazi”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *