Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, limelalamikia tabia ya baadhi ya Watendaji na Maofisa Maendeleo ya Jamii kutowatendea haki wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa Wanawake, Vijana na Makundi Maalum.
Wakizungumza katika kikao Cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika Wilayani humo, Madiwani hao wamesema kuna upendeleo kwa baadhi ya vikundi huku vingine vikikosa fursa hiyo, ambapo Wameiomba Serikali kulifuatilia suala hilo kwa ukaribu na kuchukua hatua stahiki.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo amekanusha madai ya upendeleo, na kusema kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa uelewa kwa baadhi ya wanavikundi ambao hushindwa kuwasilisha maombi yao kwa njia sahihi kupitia mfumo rasmi.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semendu, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Abubakary kuuli pamoja na idara husika, kuhakikisha wanajifunza mbinu bora za kuwapa wananchi maelezo yanayoeleweka juu ya mchakato wa kupata mikopo hiyo.


