Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Baraza la Madiwani wa Halimashauri ya Wilaya ya Kishapu limeidhinisha jumla ya shilingi bilioni 54.3 kama makisio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 2.8 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Halimashauri ya Kishapu Josephat Limbe, amewapongeza madiwani kwa kujadili kwa kina randama ya bajeti hiyo kuanzia ngazi ya kamati za kudumu,na katika vikao vya vyama vya siasa kabla ya kuidhinishwa rasimi na baraza.

Aidha, Mwenyekiti Limbe amesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa mapato yandani ili kuhakikisha miradi na mipango yote ya maendeleo katika halimashauri hiyo inatekelezwa na kutoa wito kwa madiwani wote kusimamia ipasavyo mapato katika kata zao.
“Nawasihi Waheshimiwa Madiwani kushiriki kikamilifu katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ndani ya kata zenu ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli zote za halmashauri na miradi ya maendeleo,” amesema Limbe.

Kwa upande wake, Muwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni afisa serikali za mitaa Fabian Kamoga amesisitiza umuhimu wa nidhamu katika usimamizi wa mapato na kueleza kuwa mafanikio ya bajeti hiyo yanategemea ukusanyaji wa mapato na matumizi sahihi ya fedha zitakazokuwa zimepatikana.
Naye mkurugenzi Mtendaji wa halimashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, amewapongeza wataalamu kwa kuandaa bajeti hiyo kwa weledi, na kuwataka madiwani kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii ikiwemo kuhamasisha uandikishaji wa watoto wa shule ya awali na kidato cha kwanza, pamoja na uhamasishaji wa Bima ya afya kwa wote na utambuzi wa Kaya zisizo na uwezo ili ziweze kunufaika na mpango wa kugharamiwa na Serikali.

Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatarajiwa kuimarisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kuboresha huduma za kijamii na kuendeleza miundombinu, hatua ambayo inalenga kuinua ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Kishapu katika mwaka wa fedha ujao.