MADIWANI FUATILIENI, TOENI TAARIFA ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA WANANCHI – DC FAUZIA

Na Saada Almasi, Meatu – Simiyu.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, wametakiwa kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa utoaji wa taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi katika kata zao ili wananchi hao wajue ni namna gani fedha ambazo wamezichanga kwa ajili ya shughuli za maendeleo zilivyotumika.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Fauzia Hamidu wakati wa Baraza la madiwani lililoketi mjini Mwanhuzi na kusisitiza kuwa ofisi yake imekuwa ikipokea maombi mengi ya vibali vya kuchangisha wananchi na baada ya kutoa vibali hivyo kinachofuata ni barua za wananchi kumuita kwenye mikutano huku agenda kuu ni malalamiko yao juu ya kutopewa taarifa za mapato na matumizi.

“Tunakaa kwenye viko tunaandika mihtasari tunaomba vibali kwa mkuu wa wilaya vya kuchangisha wananchi na ofisi yangu inatoa lakini sasa zile pesa zinapopatikana hakuna sehemu ambayo inaainisha matumizi ya zile pesa kwa wananchi, mnapoacha kuwapa taarifa ya mapato na matumizi mnasababisha watu kuwa na maswali ambayo yangeepukika endapo mngetimiza wajibu wenu,” amesema DC Fauzia.

Ameongeza kuwa, “na hizo pesa mnazokusanya zitumike ipasavyo kulingana na lengo la michango kama ni milioni 45 zimekusanywa kujenga zahanati zitumike pesa vizuri lakini sasa kuna ujanja ujanja mwingi mtapata milioni 45 zitakazotumika ni milioni 30 zingine mtasema mara mmelipa vibarua au mmechotea maji ya ujenzi yaani vitu ambavyo havina msingi ,niwaambie wananchi si wajinga wanafuatilia kila kitu watendeeni haki ili mzidi kujiweka mahali salama,” amesema DC Fauzia.

Sambamba na hilo Fauzia amesisitiza juu ya uhamasishaji wa wazazi kutoa michango ya chakula shuleni hasa kipindi hiki cha mavuno ili watoto wapate muda mwingi wa kujisomea wakiwa na uhakika wa kupata chakula .

“Kipindi cha nyuma watu wanalima niliwaambia mnapowalazimisha sana kutoa vyakula ni kama kuwakamua na kuwaumiza nendeni nao taratibu lakini sasa watu wanavuna mazao mengi tunayaona yameiva huu ndio wakati wa kuwahamasisha watoe hiyo michango ,ongezeni bidii ninaimani chakula cha kutosha kitapatikana ili hawa watoto kabla hatujawadai matokeo mazuri tuwe tayari tumewawekea mazingira mazuri ya kusoma,” alisema DC Fauzia.

Pamoja na mengi aliyoyasisitiza DC Fauzia pia amegusia suala la ukusanyaji wa mapato ya halmashauri kwani kwa kiasi kikubwa hutumika katika kuendeshea shughuli mbalimbali za kimaendeleo  ndani ya halmashauri hiyo.

“Mnajisifia mna makusanyo mazuri ya mapato ya halmashauri lakini ukweli ni kwamba bado hayaridhishi ,hebu tumieni njia mbadala katika maeneo yote watambue wanawajibu wa kutoa ushuru kwenye soko letu wafanyabiashara wamejaa wasingeongezeka kama hakuna mzunguko ,huko minadani vilevile lakini sasa angalieni nini mnaleta hizi njia mnazotumia badilisheni  watu wajue wajibu wao na walipe ushuru?,” aliuliza DC Fauzia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *