Na Clavery Christian Bukoba – Kagera.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba limekutana kujadili taarifa za maendeleo ya kata, huku likiweka msisitizo mkubwa katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Meya wa Manispaa ya Bukoba, Acton Rwankomezi amesema ukusanyaji wa mapato ni nguzo muhimu katika kuendesha shughuli za maendeleo, akibainisha kuwa bila mapato ya kutosha, halmashauri itashindwa kutekeleza kikamilifu mipango iliyokusudiwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Rwankomezi, amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa ya Bukoba Ndugu Jaccobo Nkwera pamoja na wataalamu wake kuhakikisha wanabainisha na kuvifikia vyanzo vyote vya mapato, ikiwemo vile ambavyo havijatumika ipasavyo, ili kuongeza mapato na kuimarisha uchumi wa halmashauri hiyo.
Aidha, Meya Rwankomezi amesisitiza umuhimu wa kudhibiti uvujaji wa mapato kwa kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi na uwajibikaji kwa watumishi, ili kuhakikisha kila fedha inayokusanywa inatumika kwa manufaa ya wananchi.

Nao baadhi ya madiwani wameitaka halmashauri kuimarisha ushirikiano kati ya wataalamu na viongozi wa kata, wakieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kubaini vyanzo vipya vya mapato na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji.
Kikao hicho kimewakutanisha madiwani kutoka kata zote 14 za manispaa ya bukoba ambao waliwasilisha taarifa zinazoonesha hali ya utekelezaji wa miradi katika sekta za elimu, afya, miundombinu na huduma za kijamii, pamoja na changamoto zinazokwamisha maendeleo katika maeneo yao.



