MADIWANI 1,697 VITI MAALUM WAPIGIWA KURA BARIADI

Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.

Katika kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Wajumbe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), wapatao 1,697 wamepiga kura kuwachagua Wagombea wa Udiwani wa Viti Maalum wa Tarafa nne Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.

Uchaguzi huo, ambao umefanyika kwa uwazi katika viwanja vya Bariadi Alliance Wilayani humo, umesimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Vicent Naano pamoja na msaidizi wake ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Busega, CDE Ngofilo.

Awali, akizungumza na Jambo fm Mwenyekiti wa Umoja huo Wilaya ya Bariadi, Getruda Ngokolo amesema hatua ya uchaguzi wa Madiwani Viti Maalumu ni kubwa kwani wao ndio wanaoandaliwa kuingia katika uchaguzi mkuu

“Hili ni jeshi kubwa sana katika Uchaguzi Mkuu ujao na tunachokifanya hapa ni kutengeneza daraja la ushindi maana idadi kubwa iliyojitokeza hapa itakuwa balozi wa kuhamasisha wananchi wengine kupiga kura” amesema Ngokolo.

Naye mjumbe kutoka kata ya Nkololo Helena Ipabaja ameuchukulia uchaguzi huo kama uhamasishaji wa kura za kumchagua rais wa jamhusi ya muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

“Idadi hii ya akinamama waliojitokeza leo tunaamini tukimaliza hapa tutajipanga zaidi maana wanawake ahadi zao huwa za kweli na nina imani tutapata kura za kishindo ifikapo uchaguzi mkuu” amesema Helena.

Hatma ya uchaguzi huo imepatikana majira ya usiku ambapo msimamizi mkuu wa uchaguzi huo ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Maswa Vicent Naano alitangaza washindi na kusema kuwa huo ni mwanzo tu kwani waliopita bado wanafursa ya kupigiwa kura ili mmoja aongoze

” niwaambie tusiende kushangilia kwa sherehe kubwa huko nyumbani tambueni kuwa huu uchaguzi unafuatiwa na mwingine utakaompa kura mmoja kati ya hapa kwa hiyo muende kujipanga isipokuwa niwapongeze kwa namna ya kipekee mmeonyesha ukomavu wa kisiasa maana kuna wagombea hapa kura zao hazipishani kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho maana yake ni kuwa wote wana hadhi ya kuwa viongozi nawapongeza sana,” amesema Naano.

Kadhalika katibu wa umoja wa wanawake wilaya ya Bariadi Angel Adam Simwanza amesema kuwa uchaguzi huu umeleta wagombea wapya na washindi wapya hii ni kudhihirisha kuwa wanawake wameamka na kupata motisha kuwa chama hakitoi nafasi kwa upendeleo.

” wanawake sasa tunakimbilia 50 kwa 50 na hii sapoti tunaipa kutoka nyumbani na hata kwa wanaume ndiyo maana umeona huu mwamko na hivi sasa tunapata wagombea wapya wengi na washindi wapya kwa asilimia 40 haya ni mafanikio makubwa ndani ya chama na kuonyesha kuwa hakuna upendeleo ndani ya chama” amesema Angel.

Jumla ya wanawake 1697 waliopiga kura walitoka katika tarafa ya Ntuzu,Nkololo,Ngulyati na tarafa ya Dutwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *