Chama cha Madaktari Bingwa wa Macho na Wataalamu wa Macho Tanzania kimefanya mkutano wake wa sita wa kitaifa, ukiwa ni jukwaa la kuimarisha huduma za macho huku pia ukiwa na lengo la kujadili mawasilisho ya tafiti mbalimbali za macho wanazozifanya hapa nchini.
Mkutano huu, ambao ulianza siku ya jana tarehe 19 Juni 2025 na kuendelea tena 20 Juni 2025, unatambulisha mada inayosema“Public‑Private Partnerships for Eye Health: Driving Sustainable Impact in Tanzania,” na umewaunganisha madaktari bingwa, wataalamu, wasomi na wadau kutoka sekta ya macho.

Akizungumza katika mkutano huo Rais wa Chama hicho Dkt. Christopher Evarist amesema kuwa changamoto ya macho hapa nchini bado ni kubwa na wanaamini kupitia mkutano huo utakwenda kua chachu ya kubadilishana uzoefu, kujadili matokeo ya tafiti, na kupanga mikakati ya kupima, kutibu na kuzuia magonjwa ya macho kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine Dkt. Christopher amewaasa wananchi kufanya vipimo vya macho mara kwa mara hata kama mwananachi hana dalili kwani tatizo la macho halina muda wala umri maalumu.

Kwa upande ake mgeni Rasmi wa mkutano huo ambae pia ni mdau mkubwa wa tiba ya macho, Lias Habil Khanbhai amewaomba wadau mbalimbali wa maendeleo hapa nchini kujitokeza ili kutoa msaada wa huduma ya macho pamoja na magonjwa mengine yanayowakabili wananchi hapa nchini.
Mtaalamu wa macho kutoka halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, Joash Lucian amesema kupitia mkutano huo wanatarajia kupata elimu zaidi juu ya taaluma ya macho pia yeye kama mhudumu anayo nafasi kubwa ya kutoa elimu na kuhamasisha wanajamii kupima macho lakini pia kuwashauri wasitumie dawa ambazo hasijaelekezwa na madaktari au wataalamu wa macho.

Nae Mtaalamu mwingine wa macho George Mauzen amesema wananchi wengi hapa nchini hawana elimu ya kutosha kuhusu afya ya macho hivyo akatoa ushauri kuwa mwananchi anapohisi kuwa na changamoto ya macho asiende kununua dawa bila kujua kiundani tatizo bali anapaswa kwenda hospitali kukutana na wataalamu ili kupata tiba stahiki ya macho.
Mkutano huo umefanyika kwa siku mbili na umehudhuriwa na wageni kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania, DR Congo, Marekani, Afrika Kusini pamoja na mataifa mengine.
