Baraza la Madaktari Tanganyika limewatia hatiani na kuwapa adhabu madaktari Tisa kwa makosa ya ukiukwaji wa kanuni za maadili na utendaji wa kitaaluma na kutoa maamuzi dhidi ya wanataaluma hao kupitia Kikao cha Baraza la Madaktari Tanganyika kilichokaa kati ya tarehe 22 hadi 26 Januari 2024 lililosikiliza jumla ya mashauri Tisa.
Hayo yamebainishwa leo Februari 9, 2024 na Mwenyekiti Baraza la Madaktari Tanganyika Prof. David Ngassapa akiwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu mashauri ya Kitaaluma yaliyowasilishwa mbele ya Baraza hilo Januari 2024.

Miongoni mwa adhabu zilizotolewa ni pamoja na kufutiwa usajili, kufungiwa leseni ya kutoa huduma kwa muda kati ya miezi sita hadi wa miaka Miwili, kupewa onyo au karipio kali na pia walielekezwa kwenda kwenye mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa mteja ya Wizara ya Afya kwa muda wa miezi sita kwa gharama zao.