Na Gideon Gregory, Dodoma.
BARAZA la Verterinari Tanzania (VCT) limewafutia usajili Madaktari wa mifugo 120 kwa kosa la kulimbikiza madeni kwa muda mrefu hivyo kukosa sifa ya utoaji huduma ya afya ya mifugo.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini hapa Dodoma leo Januari 8,2025 Msajili Msaidizi wa Baraza la Veterinari Tanzania Dk.George Mtinda ametaja sababu ya kufuta usajili huo kuwa ni kushindwa kulipa ada sh. 30,000 kwa mwaka.
“Kikao cha baraza kiliidhinisha madaktari 120 kufutiwa usajili kwa kukosa sifa za utoaji huduma ya afya ya mifugo baada ya kulimbikiza madeni kwa muda mrefu,”amesema.
Ameongeza kuwa wale waliofutiwa usajili wanaweza kuomba tena kwa kulipia faini, ada na malimbikizo ya madeni waliyokuwa wanadaiwa kabla huku akiongeza kuwa endapo watakaa nje kwa muda wa miaka miwili watatakiwa kufanya na mitihani upya ili wasajiliwe upya.
Kwa mujibu wa Dk.Mtinda amesema ulipaji wa ada ni takwa la kisheria linataka madaktari hao kuhuisha usajili kila mwaka.
Katika hatua nyingine amesema hadi sasa baraza limesajili madaktari zaidi ya 1,200 na wanaendelea kuongezeka kila mwaka.
“Kwa wale waliofutia usajili hawataruhusiwa kuendelea kutoa huduma na watakaokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani,”amefafanua.
Ameongeza kuwa:”Ni kweli kufutwa kwa madaktari hao kutasababisha upungufu wa kada hiyo lakini hatuna jinsi kwababu ni takwa la kisheria. Na Mtu anayefanyakazi bila kibali maalumu ni kishoka na hawezi kutambulika na baraza,”.
Amesisitiza kuwa baraza linawataka madaktari wa mifugo kufanya usajili kwa mujibu wa sheria ili kuondoa mgongano usio na ulazima.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Madaktari wa Wanyama Tanzania, James Kawamala, amesema hatua hiyo imesikitisha na ina athali lakini serikali imetimiza wajibu wake.
Amesema serikali imekuwa ikiwakumbusha mara kwa mara na chama kimekuwa kikitekeleza jukumu lake la kuwakumbusha wanachama wake lakini kumekuwa na uzembe.
“Kama chama tunaendelea kuhamasisha kulipa madeni ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kujitokeza ikiwemo kufungiwa huduma na kupelekwa mahakamani,”amesema.