Ikiwa zimepita siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amwagize Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Sulemani Jafo kuandaa mpango maalumu wa kuwatafutia nafasi wafanyabiashara wadogo (machinga) ili waondoke katika maeneo ya barabara, hii leo wafanyabiashara hao wadogo maarufu kama Machinga katika eneo la Buhongwa wamefanya vurugu dhidi ya askari wa akiba ‘Mgambo’ ambao wamefika katika eneo hilo ili kuchukua matunda yao.
Wafanyabiashara hao walianza kumshambulia askari huyo hali iliyomfanya akimbilie katika kanisa Katoliki Kigango cha Buhongwa ili kunusuru maisha yake.
Akielezea tukio hilo Ofisa Mtendaji wa Kata ya Buhongwa, Pily Naman amesema baada ya kupata taarifa za vurugu hizo, alifika eneo hilo akiwa na mgambo wa kata ili kuimarisha ulinzi ili machinga wasivunje uzio wa kanisa hilo.
Aidha Pily amesema kufuatia uwepo wa vurugu hizo hali hiyo ilimlazimu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana (OCD) Virginia Sodoka kufika katika eneo hilo akiwa na gari la polisi iliyokuwa na askari wenye silaha, na walizingira uzio wa kanisa hilo kisha kumchukua Mgambo huyo licha yao kushambuliwa kwa mawe.
Baadhi ya Wafanyabiashara katika eneo hilo akiwemo Abdallah Mohammed amesema, askari hao walifika sokoni hapo majira ya asubuhi na kuanza kuchukua matikiti na nanasi za wafanyabiashara, ndipo Wamachinga wengine walipomzingira mmoja wao na kuanza kumpiga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Said Tembo amesema mara kadhaa wamekuwa wakifikisha maombi yao kwa viongozi wa serikali kuwapatia maeneo yenye msongamano wa watu ikiwa ni pamoja na kufunga kwa muda baadhi ya barabara ili kuwasaidia kufanya biashara zao lakini mawazo hayo yamekuwa hayafanyiwi kazi.