Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekutana na wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga jijini Dar es Salaam na kuafikiana kiwango cha kodi kwa kundi hilo ambalo limesema lipo tayari kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Meneja wa TRA Mkoa wa Kikodi Kariakoo, Kabula Mwemezi amesema baada ya kutoa elimu ya mabadiliko ya sheria za kodi zilizopitishwa na Bunge la Bajeti Juni mwaka huu, wamachinga wamekubali kulipa Sh. 100,000 kwa mwaka.
Amesema kodi hiyo inalipwa kwa awamu nne ndani yam waka husika na itawahusu wamachinga wenye mzunguko wa mauzo ya Sh. 4,000,000 na zaidi.
Awali akifungua mafunzo hayo, Kaimu Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Edmund Kawamala, amesema wananchi wa ngazi zote wanapaswa kulipa kodi ili nchi iweze kutoa huduma muhimu zenye ubora kwa wananchi kama elimu, afya, maji na miundombinu.