Jeshi la Polisi Mkoani Rukwa kupitia kikosi cha usalama barabarani limeyazuia mabasi saba ya abiria kuendelea na safari za mikoani baada ya kukutwa na changamoto katika mifumo mbalimbali.
Mwanasheria wa kikosi cha usalama barabarani nchini Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Deusi Sokoni, akizungumza Leo Disemba 28,2023 baada ya zoezi la ukaguzi wa magari, upimaji wa kilevi na utoaji elimu ya usalama barabarani kwa madereva na abiria katika stendi ya Katumba, amesema jumla ya mabasi 25 yamekaguliwa ambapo kati ya mabasi hayo saba yamekutwa na changamoto katika mifumo na hivyo kuzuiliwa kuendelea na safari.
Mabasi yaliyozuiliwa ni pamoja na kampuni ya Ruchoro Express, Mbinga One express, Mwakamboja, MM8, Bubele trans, Mwasi express, Msigwa trans, yanayofanya safari ndefu kwenda mikoa mbalimbali nchini.