Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, amezitaka halmashauri kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika kwa wakati kuelekea ugawaji wa vyandarua 59,602 vyenye dawa katika shule za msingi 517 za halmashauri za Igunga, Sikonge, Urambo na Uyui.
Bi. Mtondoo ametoa maelekezo hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha Uraghabishi wa Zoezi la Ugawaji wa Vyandarua Mashuleni, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtemi Isike Mwanakiyungi, mkoani Tabora.

Amesema “ugawaji wa vyandarua pekee hautoshi bila kuhakikisha vinawafikia walengwa na kutumiwa kwa usahihi.”
Hivyo kuwataka viongozi wa jamii, walimu, wahudumu wa afya na vyombo vya habari kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulala kwenye vyandarua kila usiku, hususan watoto na makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kupata malaria.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Rogath Mboya, amepongeza juhudi za Serikali na wadau katika mapambano dhidi ya malaria, akieleza kuwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa zimeanza kuonesha matokeo.
Amewataka wadau zaidi wa ndani na nje ya nchi kuongeza nguvu katika mapambano hayo.

Dkt. Mboya pia amezitaka halmashauri kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya afua za kudhibiti malaria, ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kuutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
“Malaria haiathiri afya pekee, bali pia husababisha utoro shuleni, kupungua kwa tija katika familia na kuongezeka kwa gharama za matibabu.” Amesisitiza Dkt. Mboya.

Mwakilishi wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya, Bw. Gitanya Peter, amesema halmashauri za Igunga, Sikonge, Urambo na Uyui zimepewa kipaumbele kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi pamoja na kiwango kidogo cha upatikanaji wa vyandarua katika jamii.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza afua nyingine, zikiwemo unyunyiziaji wa viuadudu kwenye mazalia ya mbu, utoaji wa dawa kinga kwa wajawazito na kuhakikisha dawa za malaria zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya.



